Wednesday, 27 June 2012

Penzi ni kama kohozi

Hadija ninakuita, naomba uniitike
Kukupenda sitosita,  hata kinipiga teke
Nilini n’takupata,  nikuite wangu mke
Penzi ni kama kohozi, kulificha sitoweza

Ni weye nishaamua, mwengine sitompenda
Kila mtu kwa mtaa, yuajua nakupenda
Kupitiya i sanaa, naapa sitokutenda
Penzi ni kama kohozi, kulificha sitoweza

Alokupa u urembo, kakupa pia tabia
Sitoboi yote mambo, mengineyo takwambia
Linaua hilo umbo, bayana nawaambia
Penzi ni kama kohozi, kulificha sitoweza

Niurumie nakuomba, moyo upate tulia
Tuianze yetu nyumba, daima kufuraia
Tumshukuru Muumba, aweze kutujalia
Penzi ni kama kohozi, kulificha sitoweza

Naakika tanikithi, na jina langu ni hili
Kaburu wa Kariithi, Aderea ndo la pili
Mtungaji mwenye haathi, nayependa wana wali
Penzi ni kama kohozi, kulificha sitoweza

Sunday, 20 May 2012

Wakati umewadia

Uwanjani najitoma, jameni nipokeeni
Ni mengi lonisukuma, nafasi kuwaombeni
Vijana tunalalama, sie tuko mashakani
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
 
Viongozi chipukizi, watuita mahasidi
Tufanyeni uamuzi, katu tusikaidi
Waache hao wapuzi, walojaa ufisadi
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
 
Huu ni wakati wetu, vijana kujitokeza
Piganie haki zetu, tuwaonyeshe twaweza
Tulinde ujana wetu, mie ninawahimiza
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
 
Taratibu taratibu, tutafika kileleni
Nauliza mnijibu, kesho itafika lini?
Tuwang'atue mababu, walio mamlakani
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
 
Tamatino nimefika, lilobaki ni vitendo
Twafaa kujumuika, kimawazo na mwenendo
Rabuka tupe baraka, tujalie na upendo
Wakati umewadia, vijana tugutukeni