Uwanjani najitoma, jameni nipokeeni
Ni mengi lonisukuma, nafasi kuwaombeni
Vijana tunalalama, sie tuko mashakani
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
Viongozi chipukizi, watuita mahasidi
Tufanyeni uamuzi, katu tusikaidi
Waache hao wapuzi, walojaa ufisadi
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
Huu ni wakati wetu, vijana kujitokeza
Piganie haki zetu, tuwaonyeshe twaweza
Tulinde ujana wetu, mie ninawahimiza
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
Taratibu taratibu, tutafika kileleni
Nauliza mnijibu, kesho itafika lini?
Tuwang'atue mababu, walio mamlakani
Wakati umewadia, vijana tugutukeni
Tamatino nimefika, lilobaki ni vitendo
Twafaa kujumuika, kimawazo na mwenendo
Rabuka tupe baraka, tujalie na upendo
Wakati umewadia, vijana tugutukeni